Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo anatarajia kuanza Ziara ya kiserikali ya siku tatu kuanzia 07,Mei,2025,nchini Tanzania kufuatia mwaliko wa Rais wa Tanzania,Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,Ikulu Sharifa Nyanga imeeleza Mhe.Daniel Chapo akiwa nchini Tanzania atafanya mazungumzo rasmi na Rais Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kushuhudia uwekaji saini Mikataba na Hati za Makubaliano (MOU) katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano.
Vile vile, Rais Chapo atapata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika na mradi wa kimkakati wa Reli ya kisasa (SGR) kujifunza na kuangalia fursa za ushirikiano baina ya Tanzania na Msumbiji.
Aidha, Ziara hii itadumisha mahusiano yaliyopo, kuimarisha ushirikiano wa kisekta na kufungua fursa mpya zenye maslahi kwa nchi zote mbili.
Pia katika ziara hiyo nchini, Rais Chapo atapata fursa ya kutembelea Zanzibar ambapo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi,Mhe.Dkt. Hussen Ali Mwinyi na kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu na Soko la Samaki la Malindi.
Tanzania na Msumbiji zina uhusiano wa kihistoria na kidugu ulioasisiwa na Waasisi wa
nchi hizi mbili wakati wa ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika, Baba wa Taifa
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa FRELIMO Hayati
Eduardo Chivambo Mondlane na Rais wa kwanza wa nchi hiyo Hayati Samora Moisés
Machel.
Rais Chapo alishinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi desemba mwaka 2024 kwa jumla ya asilimia 65.7 ya kura zote zilizopigwa,na hii ni ziara yake ya kwanza ya kiserikali nchini Tanzania