Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imeeleza kuwa Ndugu Luhaga Joelson Mpina na Ndugu Fatma Abdulhabib Ferej si wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Tamko hilo la Tume limezingatia uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wa tarehe 15 Septemba, 2025 uliotengua uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina aliyependekezwa na Chama hicho kugombea Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT -Wazalendo) taarifa iliyotolewa tarehe 21 Septemba, 2025, imeonesha uwepo wa Mkutano wa Uzinduzi wa Ilani ya Uchaguzi ya ACT- Wazalendo katika Makao Makuu ya Chama hicho na kufuatiwa na Mkutano wa Uzinduzi wa Kampeni za Ubunge katika Jimbo la Segerea ambapo ikibainishwa matukio yote yatahudhuliwa na wagombea nafasi ya Urais na Makamu wake.
Mkurugenzi wa Uchaguzi,Ndugu Kailima Ramadhani ameeleza kuwa kutokana na pingamizi la kugombea nafasi hizo aliyekuwa mgombea wa Kiti cha Rais na Chama cha ACT Wazalendo walijulishwa kwa barua kuhusu uamuzi huo wa Tume. Hivyo, taarifa ya chama cha ACT-Wazalendo inayoeleza uwepo wa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais siyo sahihi.
Aidha, taarifa ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Segerea, ambaye ndiye mratibu wa Ratiba za Kampeni za Ubunge, inaonesha kuwa hakuna ratiba ya kampeni za mgombea ubunge wa Chama cha ACT- Wazalendo katika eneo lililotajwa katika taarifa ya ACT- Wazalendo.
Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imekitaka Chama cha ACT Wazalendo kizingatie masharti ya Kanuni ya 35 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 inayohusu utaratibu na ratiba za kampeni za ubunge.
