Mashirikiano ya pamoja baina ya wadau wa afya nchini yatasaidia kuleta mabadiliko ya huduma za afya kwa wagojwa wanaoishi na maradhi ya kuambuzi pamoja na maradhi yasioambukiza.
Mkurugenzi wa Tanzania Health Promotion Support THPS Dr Redempta Mbatia ametoa kauli hiyo katika mkutano ulijadili masuala ya afya unaofanyika katika viwanja vya Maonyesho Nyamanzi wilaya ya Magharibi B Unguja.
Amesema wamebaini kuwa wagonjwa wanaishi na maradhi ya kuambukizi pia wamekuwa wakipatwa na maradhi yasioambukiza hivyo ni vyema wanapohudhuria vituo vya afya kufanyiwa uchunguzi wa maradhi yasioambukiza ili kupata huduma kwa pamoja ili kupunguza gharama za matibabu.
Amefahamisha kuwa baadhi ya wagonjwa wanaoishi na HIV wanaofika vituo vya afya wamegundulika kuwa na maradhi yasiombukiza hivyo wakipatiwa huduma kwa pamoja itapunguza usumbufu kwao pamoja na kupatiwa huduma kwa wakati.
Nae Katibu mkuu wa chama cha kisukari Tanzania na katibu wa chama cha maradhi yasioambukiza Tanzania Professa Kaushik Ramaiya amesema ili kukabiliana na maradhi yasioambukiza ni lazima kutilia mkazo suala la kinga kwa wananchi.
Amesema ni vyema kwa jamii kuachana na matumizi ya sigara, pombe, ulaji, mbaya na kufanya mazoezi kwa lengo la kupunguza maradhi yasioambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu na saratani ambayo yanaongezeka kwa kasi hapa nchini.
Mkutano huo umeandaliwa na Tanzania Health Promotion Support kwa ufadhili wa shirika la Marekani la US CDC kupitia shirika la PERFAR una lengo la kijadili njia bora za kutoa huduma kwa wagonjwa wanaoishi na maradhi ya kuambukiza pamoja na yasiombukiza kwa lengo la kupunguza gharama za matibabu.