Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano kati ya Wizara ya Madini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Makubaliano hayo ni mwendelezo wa ushirikiano uliopo baina ya wizara hizo mbili zilizopo katika upande wa Muungano ikiwa ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Februari, 2023 jijini Arusha ya kushirikiana kwa lengo la kufanya madini yaliyopo katika maeneo husika yaweza kuleta manufaa kwa pande zote mbili.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa ofisi ndogo ya Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam Dkt. Biteko amewataka watendaji wa wizara hizo kusimamia utekelezaji wa makubaliano
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais yalitupa dira mpya katika kuendeleza mashirikiano yetu, hivyo tulichosaini leo sio kwa ajili ya kupiga picha bali ni kwa ajili ya kazi tuliyojipatia, natamani kuona mambo tuliyosaini hapa yanakuwa mfano na yanafanyika kwa weledi kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amewataka watendaji wakuu wa pande zote mbili kusimamia masuala hayo ili yaweza kutokea huku akitaka kuanza kusimamia masuala ambayo hayahitaji rasilimali fedha kubwa ikiwemo kufanya tafiti hivyo yale yanayowezeka yaanziwe kufanyiwa kazi leo na sio kungoja.
