Jamii imetakiwa kushiriki katika kupanda na kusimamia miti inayopandwa ili kuimarisha uchumi wa kijani kwa faida ya sasa na kizazi kijavyo.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Harusi Said Suleiman huko Ofisini kwake Migombani wakati akifungua kikao cha kuwajengea uwelewa waadishi wa habari, wahariri, waandaaji vipindi, wamiliki wa mitandao ya kijamii na Jumuiya za Habari, kuhusiana na Mpango wa kuirithisha Zanzibar ya kijani.
Amesema pamoja na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali na wadau mbalimbali katika kuhamasisha upandaji na utunzaji wa misitu lakini bado uoto wa asili visiwa vya Zanzibar unaendelea kupungua siku hadi siku.
Aidha amesema kuna sababu nyingi zinazopelekea kupotea miti na misitu kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo ukuaji wa miji ambayo ujenzi wake unachukua nafasi kubwa ya ardhi kwa matumizi ya makazi, ongezeko la watu na mabadiliko ya tabianchi.
Amefahamisha kuwa, Serikali ya awamu ya nane imeanzisha mpango wa kuirithisha Zanzibar ya Kijani ili kila mtu awajibike katika kupanda na kutunza miti ya misitu na matunda kwa ajili ya kuendeleza hali ya kijani.
“Katika kuendelea kutekeleza mikakati yetu ya kuvinusuru visiwa vyetu pamoja na kupunguza kasi ya athari za mabadiliko ya tabianchi inayoikumba Dunia hivi sasa, tumekuja na Mpango huu ili kuweza kuwa muarubaini wa kutibu tatizo hili” alisema Waziri huyo.
Sambamba na hayo amesema Mpango huo utasadia kuongeza hamasa kwa kila mtu kwa kushiriki kikamilifu na kujenga jamii yenye utamaduni endelevu wa kupenda kupanda, kutunza na kuacha kukata Miti ovyo.
Hata hivyo ameiasa jamii kuweka utamaduni wa kupanda miti, kuisimamia na kuhamasisha wananchi pamoja na wadau kuona umuhimu wa kuutunza miti kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar Sheha Mjaja Juma amesema utekelezaji wa mpango wa urithi wa kijani ni shirikishi kwa kuweza kuwakutanisha wadau wote pamoja kutoka sekta na ngazi zote.
Hata hivyo amesema lengo ni kuhamasisha jamii kutumia nishati mbadala na kuacha kutumia mkaa na kuni ambayo ambazo zinasababiiiisha uharibifu mazingira hapa nchini.
Mpango wa kurithisha Zanzibar ya Kijani unatarajiwa kuzinduliwa tarehe 10 Agost.2024, katika Viwanja vya maonyesho ya kibiashara Nyamanzi Wilaya ya Magharibi B.