Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe.Riziki Pembe Juma ameelezea jukumu la kumlinda mtoto juu ya matukio mbalimbali ya ukatili sio la Serikali pekee bali ni la kila mtu wakiwemo viongozi wa dini,watendaji wa Serikali,vyama visivyo vya kiserikali (NGO’S).
Mhe. Riziki ameeleza hayo wakati akitoa Salamu kutoka Zanzibar, huku akisisitiza ushirikiano wa wadau na Serikali zote mbili katika kukemea na kupiga vita vitendo, wakati wa ziara ya Kamati tendaji ya Mradi wa “Hapana marefu yasiyo na mwisho”, katika Mkoa wa Mwanza.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inasimamia sheria ya Mtoto no 6 ya mwaka 2011 ambapo inamtambua mtoto ni kuanzia umri 0 hadi 18, na hivo kupiga vita suala zima la ndoa kwa watoto wa umri huo na yeyote anaebainika kwenda kinyume na hilo hatua kali za kisheria zimekuwa zikichukuliwa dhidi yao.
Hivyo amewaomba viongozi wa dini, watendaji wa Serikali, NGOs na wadau wote wa mradi huo kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake kuwa na jukumu la kupiga vita ndoa za utotoni, kuziangalia sheria zilizopo ili ziendane na azma nzima ya kutokomeza suala hilo na kuwaacha watoto wa kike kusoma ili kutumiza ndoto zao za baadae.
Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Mradi wa “Hapana Marefu Yasiyo na Mwisho”, Bi Patricia Mwaikenda amesema lengo la mradi huo ni kuwashirikisha zaidi viongozi wa dini mbalimbali katika kuona wanasaidia na kuielimisha jamii na kukemea ndoa za utotoni.
Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Mradi huo na Mkuu wa Kanisa Mstaafu wa KKKT, Dkt Fredrick Onael Shoo, amesema ni vyema kuchukua hatua kwa pamoja na kuleta mabadiliko chanya juu ya suala zima la ndoa za utotoni ili kuwaacha huru watoto wa kike katika masomo yao.