Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Tulia Ackson amewataka wananchi wa mkoa wa Mbeya kuendelea kutumia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa lengo la kuhakikisha wanaunga mkono Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Tawi jipya la Benki ya PBZ Mbeya amesema maendeleo yanayofanywa na Maraisi hawa wa nchi ni kutokana na sera thabiti na miongozo yao juu ya masuala ya kifedha.
Dkt Tulia Amewahimiza wananchi wa jiji la Mbeya kuitumia benki hiyo ili kujiwekea akiba na kupata fursa ya kupata mikopo itakayowasaidia kuendeleza biashara zao na kuachana na tabia ya kutumia njia za kizamani kuweka fedha ndani kwani ni hatari kwa usalama wao.
Aidha Dkt Tulia amewataka kuwa makini juu ya mikopo ya vichochoroni ikiwemo KAUSHA DAMU, kwani inahatarisha usalama wa mali zao na kuwa duni kimaisha huku akiwaahidi PBZ kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litaendelea kushirikiana na Benki hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa jamii.
Hata Hivyo Dkt Tulia ameupongeza uongozi wa Benki ya PBZ kwa kuamua kufungua Tawi hilo Mbeya mjini katika nyanda za juu kusini kwani Mkoa huo una makundi mengi ambayo yanahitaji kusukumwa kwa kupatiwa mikopo ili kujiendeleza zaidi.
Mapema Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe.Riziki Pembe Juma akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt Saada Mkuya Salum amesema, katika kuziendeleza Sera jumuishi za masuala ya kifedha, Benki ya Watu wa Zanzibar PBZ imekuwa na utaratibu wa kufungua matawi katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema PBZ ni Taasisi ya kifedha inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia mia moja chini ya Ofisi ya Rais Fedha na Mipango hivyo amesema uzinduzi wa Tawi hilo ni ishara ya kuendeleza mipango thabiti katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mhe.Riziki amewashukuru Watanzania wa makundi mbali mbali kwa kuipokea vizuri Benki hii kuifanya kuwa ni miongoni mwa benki zinazofanya biashara vizuri zaidi na kuweza kuwa na Rasilimali ya zaidi ya Trilioni mbili iliyopelekea kuwa ni miongoni mwa Benki kubwa Tanzania.
Aidha Mhe.Riziki ametumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wa makundi mbali mbali kuendelea kuudumisha na kuimarisha Muungano huu na kuiunga mkono benki ya PBZ ili iweze kufanya vizuri zaidi na kuweza kuwafikia
Watanzania wengi zaidi maeneo mbali mbali huku akiwataka waliokuwa hawajajiunga na benki hii kwani kwa sasa makundi yote yamezingatiwa kifursa wakiwemo Wafanyabiashara,Watumishi, Wajasiriamali, Wakulima, Wanawake na wengineo.
Mhe.Riziki ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi Wakuu wa Nchi, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza laMapinduzi kwa namna wanavyoendelea kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo usimamizi wa sera jumuishi za masuala ya kifedha.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya PBZ ndugu Arafat Ali Haji amesema PBZ kwa mwaka huu imepanga kufungua Matawi yake katika Mikoa ya Mwanza na Arusha ili kuendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.