Sat. Jun 14th, 2025

Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Dustan Ndunguru amewakumbusha wadau juu ya makosa yanayotendeka kimtandao na kuwa nchi ilitunga sheria mahususi juu ya makosa hayo, hivyo ni wajibu wetu kama wadau wa haki kusimama na kukemea vitendo hivi ukatili wa kijinsia.

Ameyasema hayo hivi karibuni akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, ambapo chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA), kiliandaa zoezi la Mahakama ya Mfano na kuendesha kesi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ambapo kauli mbiu ilikuwa ni “kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia mitandaoni”. Zoezi ili lilihusisha waheshimiwa majaji, mahakimu, mawakili wa serikali, mawakili wa kujitegemea, polisi, wakufunzi na wanafunzi wa vyuo vikuu Mzumbe na CUCoM mkoa wa Mbeya.

 “Nimefurahi kuona kuwa mmeshirikisha watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi na naamini zoezi ili la Mahakama ya mfano litasaidia kujua makosa ya kimitandao, mara nyingi tunajisahau na kuhisi tunafanya utani ila ni muhimu tukumbuke kuna madhara ya maneno yetu mitandaoni na ili suala limekuwa likituathiri na kama walengwa kwa pamoja tusimame kupinga unyanyasi na ukatili wa kijinsia. Tuelimike lakini pia tuielimishe jamii inayotuzunguka” alisema jaji Ndunguru

Pia alishukuru TAWJA, Mahakama ya Tanzania na washiriki wengine wote kwa kuona umuhimu wa kushiriki katika maadhimisho hayo ya kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Aidha uongozi wa TAWJA Mbeya ulisimamia na kuendesha zoezi ilo la Mahakama ya mfano ikiwa washiriki katika Mahakama hiyo wakiwa ni Mahakimu, Mawakili wa serikali, Mawakili wa kujitegemea, mapolisi pamoja na wanafunzi.