Sun. Jun 15th, 2025

Na Mozah Salum

Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imekanusha taarifa iliosambaa katika baadhi ya mitandao ya kijamii  ya kusafirishwa wanyamapori hai kwa ndege kubwa kwenda moja ya nchi ya falme za kiarabu kwa kutumia ndege kubwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na NCAA na kusainiwa na Kaimu Meneja kitengo cha uhusiano wa umma bw Hamis Dambaya imesema taarifa hizo hazina ukweli wowote na zinapaswa kupuuzwa.

“Mamlaka zinazosimamia ulinzi na uhifadhi wa wanayamapori hai katika eneo lote la Loliondo zimethibitisha kuwa hakuna zoezi lolote linalohusu ukamataji wa wanyamapori hai katika eneo hilo” imeeleza taarifa hiyo.

Mwaka 2016 serikali ilitoa katazo ama zuio la ukamataji na usafirishaji wa wanyamapori nje ya nchi ambapo katazo hilo halijawahi kutenguliwa na serikali na hakuna kibali chochote cha ukamataki wa wanyamapori hai kilichotolewa. 

Kwa sasa serikali kupitia mamlaka uhifadhi wa eneo la Ngorongoro inasisitiza mwendelezo wa kusimamia shughuli za ulinzi na uhifadhi kwa kuzingatia misingi ya sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Inafahamika kwamba eneo la Loliondo halina kiwanja cha ndege kinachoruhusu ndege kuruka na kutua nyakati za usiku kama taarifa hiyo ya upotoshaji ilivyoeleza.