Sun. Jun 15th, 2025
Mkurugenzi wa Tume ya Ukimwi Zanzibar(ZAC) Dr Ahmed Mohamed Khatib akizungumza katika mkutano wa Jumuia ya Wajane Zanzibar kwa Wafanyabiashara wajane wa Masoko ya Mombasa na Jumbi,Unguja

Taasisi za Serikali na binafsi zimeombwa kushiriki juhudi za kuwawezesha wajane kliuchumi zinazofanywa na Jumuia ya Wajane Zanzibar (ZAWIO).

Wito huo umetolewa na Jaji wa Mahakama kuu Zanzibar Mhe. Fatma Hamid Mahmoud wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya Wajane wanaofanya Biashara katika Soko la Jumbi na Mombasa Unguja ili kuweza kuendesha biashara zao kwa ufanisi.

Alisema Mashirika na Taasisi nyingi zinatoa kipambele zaidi kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na kulisahau kundi la Wajane ambalo linahitaji kusaidiwa kwa kiasi kikubwa.

Aidha alisema pamoja na kuwa Wajane wanaweza kuingizwa katika kundi la wanawake lakini baadhi yao wanajitegemea wenyewe na wengi wao hawana kazi za uhakika za kuwapatia kipato cha kuendeleza Maisha yao kila siku.

Hata hivyo alisema kutokana na Changamoto mbalimbali wanazozipata kuna uwezekano mkubwa wa kundi hilo kujiingiza katika mambo yasiofaa ili kukidhi mahitaji yao.

‘‘Tunajua kuna kundi la Wajane ambao wanapata matatizo ya akili kutokana na msongo wa Mawazo kwa kushindwa kukabiliana na shida za Maisha na lakini hata pia wengine kujiingiza katika masuala ya mapenzi” alisema Jaji Fatma.

Hata hivyo ameipongeza taasisi ya Wajane kwa kuanzisha program maalum za kuwasaidia kufanya shughuli za Uchumi kwa kuwaunganisha na Mabenk ili kuweza kuwapatia Mitaji.

Mapema akitoa maelezo Mkurugenzi wa Jumuia ya Wanawake Zanzibar (ZAWIO) Tabia Makeme Mohammed amesema mafunzo hayo, yamejikita zaidi kuwapatia elimu ya mbinu za kuanzisha na kuendeleza Biashara, kujua fursa zilizopo kupitia Jumuia hiyo na kujikinga na VVU na magonjwa ya Afya ya akili.

Aidha alisema mafunzo hayo pia yatawasaidia kujuwa haki zao za msingi ikiwemo taaluma juu ya Afya ya akili, Utawala wa Sheria, usawa wa vyombo vya Dola na kugombania nafasi mbalimbali za Uongozi ili kusukuma gurudumu la Maendeleo.

Wakiwasilisha mada katika Mafunzo hayo mwakilishi kutoka Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) na kutoka Hospitali ya Wagonjwa wa akili Kidongochekundu wamesema kundi la Wajane lipo hatarini kukumbwa na matatizo ya Afya ya akili na Ukimwi hivyo linapaswa kuangaliwa kama makundi mengine.

Hata hivyo walisema maradhi ya afya ya akili yanapaswa kupewa kipaombaele kama maradhi mengine kwani yamekuwa na athari kubwa katika jamii ikiwemo Ulemavu na kurudisha nyuma maendeleo.

Mafunzo hayo ya siku moja ya kuwajengea uwezo Wajane wanaofanya Biashara katika Soko la Jumbi na Mombasa, Unguja yameandaliwa na Jumuia ya Wajane Zanzibar (ZAWIO) na kudhaminiwa na Taasisi ya WCF.