Sun. Jun 15th, 2025
Baadhi ya wanachi wa Jamii ya Kimasai wakishiriki Tamasha la kimila katika eneo la Ngorongoro kreta baada ya Serikali. kutoa kibali.

Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imezitaka baadhi ya taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka ndani na nje ya nchi kuacha upotoshaji na kutafuta ukweli kuhusu zoezi la kuhamisha wananchi kwa hiari kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni Mkoani Tanga.

Kaimu meneja wa uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw Hamis Dambaya ameeleza kuwa Serikali haitumii nguvu kwa wananchi wake wanaoishi hifadhini, na imetoa kibali cha kufanyika kwa Tamasha la kimila kwa wananchi wa jamii ya kimasai katika eneo la kreta ambalo pia lilihudhuliwa na baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo.

Amesisitiza kuwa Jamii ya kimasai, wahadzabe, wamang’ati wanaoishi ndani ya Hifadhi imekuwa na ushirikiano mkubwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ndiyo maana zoezi la uelimishaji wa wananchi kuhama kwa hiyari limekuwa likifanyika bila upinzani wowote hivyo ni vema taasisi hizo kuacha kuipotosha dunia.

“Matamasha na sherehe kama hizi mamlaka huyatumia kama sehemu ya kuja kutoa elimu kwa wananchi katika njia ya makundi ama mtu mmoja mmoja na hizi ni salamu tosha kwa mashirika ya kimataifa yanayodai kuwa Tanzania inawaondoa wamasai kwa nguvu katika maeneo yao”.Kaimu Meneja huyo wa uhusiano kwa umma amesema,

Ameeleza kuwa katika Tamasha hilo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iliweza kuwaelimisha wananchi mmoja mmoja ama kwa makundi kuhusu huduma za kijamii ambazo Serikali inazitoa katika Kijiji cha Msomera ukilinganisha na maisha ya ndani ya hifadhi na baadhi ya wananchi kusema kuwa wapo tayari kuondoka katika eneo hilo kuwafuata wenzao waliotangulia.

Kauli hiyo ya kaimu Meneja wa Uhusiano kwa Umma imetolewa kuzijulisha baadhi ya Taasisi za kimataifa ikiwemo ile inayojiita Masaai International Solidarity Alliance, Kitengo cha kutetea Haki za binadamu cha Chuo Kikuu cha Pretoria na Jarida la Africa Intelligence ambapo katika siku za hivi karibuni walitoa taarifa kwamba kuna uondoaji wa kutumia nguvu wa wamasai katika maeneo yao jambo ambalo sio la kweli.

Dambaya amesema tuhuma hizo zina upotoshaji mkubwa kwani katika jamii inayozunguka nchi nzima kutafuta malisho na maeneio ya kuchungia hakuna mwananchi hata mmoja katika nchi hii aliyewahi kubughudhiwa kutoka eneo lake ama sehemu aliyoamua kuhamia.

“Tanzania hakuna sehemu ambayo jamii ya wafugaji wanasumbuliwa au kuondolewa  kwa nguvu na ndiyo maana wameenea kila kona kuanzia bara hadi visiwani sasa anapotokea mtu  na kudai kuwa mmasai anahamishwa kwa nguvu tena shirika hilo likidai ni la kutetea wamasai labda wanaoongoza shirika hilo ni wamasai wa nchi nyingine duniani lakini hawa wa hapa nchini wanaujua ukweli na hakuna mtu anayewabughudhi”.alisema Dambaya.

Katika tamasha hilo vijana wa kimasai wakiongozwa na wazee wa mila walifanya matambiko yao ya kimila ambapo walisema zoezi kama hilo hata wakiamua kuhamia sehemu yoyote ile duniani wanaweza kuendelea kulifanya bila athari yoyote ambapo pia baadhi ya wageni waliotembelea kreta waliweza kuwashuhudia jamii hiyo ikishiriki tamasha hilo.

Baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani yamekuwa yakipotosha kuhusu zoezi la kuhamisha watu kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera kutokana na wengi wa watetezi hao kusikiliza taarifa za watu wachache wanaowatumia wananchi wa jamii hiyo kuweza kupata kipato kupitia baadhi ya mashirika  yasiyo ya kiserikali  ambayo yamekuwa yakipokea fedha kwa madai ya utetezi wa haki za binadamu.

Serikali ya Tanzania inaendelea na zoezi la kuhamisha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongorowanaojiandikisha kuhama kwa hiyari ili kuweza kuwanusuru wananchi hao kutokana na ugumu wa maisha na kwenda sambamba na kutimiza malengo ya milenia yanayosisitiza juu ya usalama wa watu na maisha bora kwa wote.