Sun. Jun 15th, 2025
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi na watendaji wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii TASAF uliofika Ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kujitambulisha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amewataka watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya wananchi zinalindwa na kutumika ipasavyo ili Watanzania waendelee kunufaika na Mfuko huo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Uongozi  Mpya wa TASAF uliofika Ofisini kwake Vuga  kwa lengo la kujitambulisha.

Amesema kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  TASAF umekuwa ni mkombozi kwa Watanzania walio wengi hasa wanyonge hivyo uongozi huo una jukumu kubwa la kuhakikisha unadhibi na kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha za mfuko huo.

 Makamu wa Pili wa Rais ameutaka Uongozi huo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF  Bw,  Shedrack Mziray   kulipa kipaumbele suala la utoaji wa Taaluma kwa wanufaika juu ya dhamira na malengo ya mfuko huo ili kupunguza malalamiko kwa wanufaika hao mara tu wanapomaliza ama kukosa sifa za kuendelea kunufaika na huduma zinazotolewa na TASAF.

Aidha Mhe. Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoka mashirikiano  makubwa kwa watendaji wa TASAF wa Pande zote mbili za Muungano ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kunufaika na mfuko huo na malengo ya Viongozi wakuu wa Serikali ya kuwaondolea changamoto mbali mbali wananchi wake yanafikiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shedrack Mziray amesema atahakikisha anayafanyia kazi  maelekezo na maagizo yote waliyopatiwa na  Makamu wa Pili wa Rais kwa kuendelea kudhibiti Nidhamu katika matumizi ya fedha, Nidhamu kwa watendeji wa mfuko huo na kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo ya kuwepo kwa mfuko huo nchini.

Mziray amesema Tasaf inafanya kazi kwa karibu na kwa mashirikiano makubwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar hivyo anaamini kuwa  ushirikiano huo utaendelea  kudumu katika kipindi chote cha Utumishi wake na kuahidi kuwa Matunda ya Mfuko huo yatawafikia na kuwanufaisha wananchi.