Sun. Jun 15th, 2025

TIMU ya 33 ya Madaktari kutoka China, imesema, itaendelea  kuwapatia mafunzo wanafunzi wa kada ya afya wa Chuo cha Sayansi za Tiba na wataalamu wa afya ili waweze kutoa huduma bora za afya nchini.

Akitoa mafunzo juu ya saratani ya kinywa, Dk.Chu Weiming, alisema, saratani ya kinywa mara kwa mara hupita bila ya kutambuliwa hadi kufikia hatua ya juu na kwamba ugunduzi wa mapema wa dalili ni muhimu kwa ajili ya utambuzi wa haraka na matibabu.

Alisema, maumivu ya mara kwa mara ya kinywa au usumbufu ambao hauonekani kuisha ni mojawapo ya ishara kuu za onyo na hiyo inaweza kuhusisha uchungu kwenye shingo, midomo, au ulimi.

Aidha, ameeleza kuwa, saratani ya mdomo inaweza pia kuonyeshwa kwa mabadiliko yasiyoeleweka katika ulimi na rangi ya tishu za mdomo.

Pia amefafanua kuwa, hisia kama uvimbe kwenye koo au shida ya kumeza inaweza kuonyesha matatizo ya msingi.

Lakini pia zaidi ya hayo, upungufu wa pumzi unaoendelea, kupungua uzito bila ya sababu, na mabadiliko ya ubora wa sauti inaweza kuwa viashiria vya mapema vya saratani ya mdomo.

Aidha amedhihirisha kuwa , uhamasishaji ni muhimu katika vita dhidi ya saratani ya kinywa kwani utambuzi wa mapema huongeza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa matokeo ya mafanikio.

Lengo la mafunzo hayo kwa wanataaluma  ni kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya kwa kuwawezesha kujifunza  njia mpya na za kisasa za kufanya kazi.hivyo wanataaluma wa kada ya afya wanatakiwa kujenga utamaduni wa kijifunza mara kwa mara ili kudumisha kiwango cha elimu mtazamo unaotakiwa katika kutoa huduma bora za kiafya.

Kwa upande wao wanataaluma hao walisema, mafunzo hayo yatawasaidia  kujenga uwezo wao kitaaluma na kuwawezesha  kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Aidha, waliiomba serikali kuendelea kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo tofauti  ili kuifanya kada ya afya kuwa ya kisasa zaidi.

Mafunzo hayo ni miongoni mwa muendelezo wa mashirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza) kupitia Chuo cha Sayansi ya tiba za Afya na Chuo cha Taifa cha Afya cha Beijing nchini China.