Na Mwandishi wetu, Msomera Tanga.
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) inafuatilia kwa karibu ujenzi wa miundombinu ikiwemo makazi na huduma zingine za mahitaji ya binadamu kwa ajili ya wananchi wanaohama kutoka hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha kwenda kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga.

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi NCAA Jenerali Venance Mabeyo (mstaafu) amethibitisha utekelezaji wa miradi ambayo imekamilishwa kuwa ni nyumba 2500,na hatua za mwisho katika ujenzi wa huduma za Maji,Mawasiliano,Barabara,shule,zahanati,maeneo ya malisho ya pamoja,minada,kituo cha kuuzia maziwa.
“Tumetembelea eneo la Block F ambapo nyumba 1,000 zimekamilishwa katika awamu ya kwanza iliyohusisha ujenzi wa Nyumba 5,000, kitalu hiki pekee kuna matenki matatu ya maji yenye ujazo la lita laki 3 kwa kila moja, tenki lingine la ujazo wa lita laki 650,000 linajengwa, hii inathibitisha kuwa wananchi wanaopisha shughuli za uhifadhi Ngorongoro wakija hapa watafurahia maisha yao” ameongeza Jenerali Mabeyo.
Pamoja na Bodi ya Wakurugenzi NCAA, mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando amewahakikishia wananchi wa Ngorongoro wanaohamia eneo hilo kuwa hali ya usalama ni shwari, nyumba zimekamilika, huduma za kijamii zipo katika eneo lote la Msomera na huduma zingine zinaendelea kujengwa ili kukidhi mahitaji ya wananchi wanaohamia.
Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi NCAA, SACC Gloria Bideberi amesema kuwa uongozi wa NCAA utahakikisha kuwa kazi ya uelimishaji na uhamasishaji kwa wananchi inaendelea kwa kasi zaidi ili wananchi waliopo Ngorongoro waendelee kuhamia Msomera. Ameongeza kuwa kaya takribani 30 kutoka Ngorongoro zitahamishiwa katika kijiji hicho mwisho wa mwezi Novemba,2024 baada ya kukamilisha uthamini na kulipwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.