Wizara ya Maliasili na Utalii imeielekeza menejimenti ya Hifadhi ya Ngorongro (NCAA) kuendelea kutekeleza jukumu la kuwaelimisha wananchi ili wahame kwa hiari kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uhifadhi na kuboresha ustawi wa maisha yao nje ya hifadhi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameeleza kuwa zoezi la kuelimisha wananchi na kuwahamisha kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda maeneo yaliyotengwa na Serikali liko palepale.
Mhe. Dkt. Pindi ametoa kauli hiyo alipotembelea makao makuu ya ofisi za Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kuongea na Menejimenti ya NCAA na kusisitiza kuwa ili kuimarisha shughuli za ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na Misitu,Waziri Chana amezielekeza taasisi za uhifadhi kuongeza ubunifu na juhudi katika matumizi ya teknolojia za kisasa zinazoendana na wakati uliopo kwa ajili ya kuimarisha usalama wa rasilimali hizo kwa maslahi ya taifa na vizazi vijavyo.
Aidha,Waziri huyo Mhe. Balozi, Dkt. Pindi ameeleza kuwa Wizara yake itahakikisha maelekezo ya Serikali yaliyotolewa hivi karibuni kwa wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kuhusiana na uboreshaji wa huduma za jamii yanatekelezwa kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.

Akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yaliyoibuliwa na wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kati ya tarehe 18- 23 agosti, 2024, Naibu Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii (Maliasili) CP. Benedict Wakulyamba amebainisha kuwa wananchi waliandamana na kutoa madai yao katika hali ya amani na utulivu bila kuleta athari katika eneo la hifadhi ambapo pamoja na changamoto zilizojitokeza shughuli za utalii ziliendelea.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi, NCAA, Dkt. Elirehema Doriye amemwambia Mhe. Waziri kuwa utekelezaji wa shughuli za uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii zinaendelea vizuri na uongozi wa NCAA unaendelea kuboresha miundombinu ya barabara na huduma zingine kwa wageni wanaondelea kutembelea hifadhi kila siku.