Sun. Jun 15th, 2025

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekubalina na Serikali ya Saudi Arabia kuwa na akaunti mbili za pamoja chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uendeshaji wa safari za Hijja kutoka Zanzibar hadi Makkha nchini Saudi Arabia ili kupunguza gharama za Mahujaji wanaohudhuria ibada hiyo.

Makubaliano hayo, ambayo utekelezaji wake utaanza mwakani yatahusisha shirika la ndege la Saudi Arabia kwa ajili ya safari za ndege zitakazoanzia Zanzibar hadi Makkha nchini Saudi Arabia.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Hussein Mwinyi amewaeleza waumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Eid Hajj lilofanyika wilaya ya Micheweni,Mkoa wa Kaskazini Pemba huku akisisitiza umuhimu wa Hijja kuwa ni taasisi ya mafunzo na malezi,maarifa kwa waislamu na kuwa Wacha-Mungu katika kujiepusha na vitendo viovu.

Katika hatua hiyo,Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatekeleza dhamira ya uanzishwaji wa Mfuko maalum wa Hijja ili kuwasaidia waumini wa Kiislamu kutekeleza ibada hiyo,baada kupokea ripoti ya kamati ya wataalamu ya kuimarisha Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ili iendeshwe kwa ufanisi na kuleta tija zaidi ikiwemo kuanzisha na kusimamia mfuko wa Hijja.

Jumla ya Mahujaji 2087 katika 3300 kwa mwaka huu,walikwenda Makkha nchini Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hijja,huku idadi ya mahujaji kutoka Zanzibar ikiongezeka ukilinganisha na mwaka jana.Hijja ni moja kati ya nguzo tano za dini ya Kiislamu ambazo zinatakiwa kufuata kama mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W) na hufanyika Makkha Saudi Arabia,ambapo kila mwaka waislamu kote duniani hujumuika kwa ajili ya ibada hiyo