Mon. Jun 16th, 2025

Timu ya Wataalam kutoka Benki ya Dunia inayoendelea na kazi yake ya kutadhmini utekelezaji wa mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW), umevutiwa na namna Vikundi vya Kijamii vinavyowezeshwa na Mradi wa REGROW kiuchumi, kwa namna vinavyo piga hatua ya kimaendeleo kiuchumi na kiuhifadhi wa Maliasili nchini.

Akizungumza kwenye ziara ya wataalam hao, katika Kijiji cha Kisaki Kituoni, Mratibu Msaidi wa Mradi wa REGROW kutoka Benki ya Dunia Bw. Nicholas Soikan licha ya kuvipongeza vikundi hivyo, amesema lengo la Benki ya Dunia kuipatia Tanzania Mkopo wenye masharti nafuu kutekeleza Mradi huo, ni kuona watanzania wananufaika na Urithi adhimu wa Maliasili zilizopo hususani Kusini mwa Tanzania, kwa kuboresha usimamizi wa Maliasili hizo, kukuza Utalii na kuwainua wanachi kiuchumi.

Bw Soikan ameongeza kuwa nifaraja kubwa kuona na kuwasikia wananchi wakitoa ushuhuda wa namna mradi wa REGROW ulivyoweza kubadili maisha yao kiuchumi na kimtazamo wa umuhimu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere katika maendeleo ya nchi kwa ujumla, jambo linalo pelekea Wanakijiji hao kuwa sehemu ya Uhifadhi endelevu wa Hifadhi hiyo kubwa kuliko zote Duniani.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanakijiji cha Kisaki Kituoni, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho Bw. Shabani Mgohamwelu, ameeleza kuwa mradi wa REGROW umewapatia furaha wananchi na kuwa wanakijiji hicho wataendelea kuwa sehemu ya Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Nyerere kwa kuwa wameona manufaa makubwa ya kuishi jirani na Hifadhi hiyo, huku akiwaomba Wataalam hao kutoka Benki ya Dunia kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea watanzania maendeleo.

Akisoma Taarifa ya utekelezaji wa mradi wa REGROW kijijini hapo, Mwezeshahi Jamii (FC) Bi Jamillah Sinahofu Bomeza amesema kuwa, mradi wa REGROW, hadi sasa katika Kijiji cha Kisaki Kituoni vikundi 12 vyenye jumla ya wanachama 222 vimepatiwa fedha mbegu Tsh 120,930,200 na fedha kwa ajili ya miradi Tsh 234,517,301.20 huku wanafunzi 35 wakipatiwa ufadhili wa masomo.

Naye Mmoja wa wananufaika wa REGROW Bi Mwanahamisi Kichombaki ebeainisha kuwa kupitia mradi huo, ameweza kuanzisha Biashara ya Juisi, anasomesha anamudu chakula na ameweza kununua Kiwanja ambacho anatarajiwa kuanza ujenzi hivi karibuni.

Katika hatua nyingine timu ya wataalam hao kutoka Benki ya Dunia wakiwa wameambata na Watekelezaji wa Mradi wa REGROW nchini, wametembelea na kujionea hatua mbalimbali zilizofikiwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika Hifadhi ya Taifa Nyerere ukiwemo uwanja wa ndege wa Mtemere.